Waebrania 6
Swahili NT
1Basi, tusonge mbele kwa yale yaliyokomaa na kuyaacha nyuma yale mafundisho ya mwanzo ya Kikristo. Hatuhitaji kuweka msingi tena kwa kurudia yale mafundisho ya mwanzo kama vile kuachana na matendo ya kifo, kumwamini Mungu; 2mafundisho juu ya ubatizo na kuwekewa mikono; ufufuo wa wafu na hukumu ya milele. 3tusonge mbele! Hayo tutayafanya, Mungu akitujalia. 4Maana watu wanaoiasi imani yao inawezekanaje kuwarudisha watubu tena? Watu hao walikwisha kuwa katika mwanga wa Mungu, walikwisha onja zawadi ya mbinguni na kushirikishwa Roho Mtakatifu; 5walikwisha onja wema wa neno la Mungu na nguvu za ulimwengu ujao, 6kisha wakaiasi imani yao! Haiwezekani kuwarudisha watubu tena, kwa sababu wanamsulubisha tena Mwana wa Mungu na kumwaibisha hadharani. 7Mungu huibariki ardhi ambayo huipokea mvua inayoinyeshea mara kwa mara, na kuotesha mimea ya faida kwa mkulima. 8Lakini kama ardhi hiyo ikiota miti ya miiba na magugu, haina faida; karibu italaaniwa na Mungu na mwisho wake ni kuchomwa moto.

9Lakini, ingawa twasema namna hii, wapenzi wetu, tunalo tumaini kubwa juu ya hali yenu. Tunajua kwamba mmepokea baraka zile bora za wokovu wenu. 10Mungu hakosi haki; yeye hataisahau kazi mliyoifanya au upendo mlioonyesha kwa ajili ya jina lake katika huduma mliyowapa na mnayowapa sasa watu wake. 11Hamu yetu ni kwamba kila mmoja wenu aonyeshe bidii hiyohiyo mpaka mwisho, ili yale mnayotumainia yapate kutimia. 12Msiwe wavivu, bali muwe kama wale wanaoamini na wenye uvumilivu na hivyo wanapokea yake aliyoahidi Mungu.

13Mungu alipompa Abrahamu ahadi, aliapa kwa jina lake mwenyewe, maana hakuna aliye mkuu kuliko Mungu ambaye kwa huyo angeweza kuapa. 14Mungu alisema: "Hakika nitakubariki na nitakupa wazawa wengi." 15Abrahamu alisubiri kwa uvumilivu na hivyo alipokea kile alichoahidiwa na Mungu. 16Watu wanapoapa, huapa kwa mmoja aliye mkuu zaidi kuliko wao, na kiapo hicho husuluhisha ubishi wote. 17Naye Mungu aliimarisha ahadi yake kwa kiapo; na kwa namna hiyo akawaonyesha wazi wale aliowaahidia kwamba hatabadili nia yake. 18Basi, kuna vitu hivi viwili: ahadi na kiapo, ambavyo haviwezi kubadilika na wala juu ya hivyo Mungu hawezi kusema uongo. Kwa hiyo sisi tuliokimbilia usalama kwake, tunapewa moyo wa kushikilia imara tumaini lililowekwa mbele yetu. 19Tunalo tumaini hilo kama nanga ya maisha yetu. Tumaini hilo ni imara na thabiti, nalo lapenya lile pazia la hekalu la mbinguni mpaka patakatifu ndani. 20Yesu ametangulia kuingia humo kwa niaba yetu, na amekuwa kuhani mkuu milele, kufuatana na utaratibu wa ukuhani wa Melkisedeki.



Public Domain Swahili New Testament -- PLEASE MAKE COPIES FOR YOUR FRIENDS, NO ROYALTY DUE.

Bible Hub

Hebrews 5
Top of Page
Top of Page