Waefeso 2
Swahili NT
1Ninyi mlikuwa mmekufa kwa sababu ya makosa na dhambi zenu. 2Wakati ule mliishi kufuatana na mtindo mbaya wa ulimwengu huu, mkawa mnamtii mtawala wa pepo wenye nguvu wa anga, pepo ambao huwatawala sasa watu wasiomtii Mungu. 3Na hata sisi sote tulikuwa kama wao; tuliishi kufuatana na tamaa zetu za kidunia na kufanya tu mambo yale yaliyoipendeza miili na akili zetu. Kidunia, sisi kama vile pia wao, tulistahili ghadhabu ya Mungu. 4Lakini Mungu ni mwenye huruma nyingi. Alitupenda kwa mapendo yasiyopimika, 5hata, ingawa tulikuwa tumekufa kwa sababu ya dhambi, alitufanya hai pamoja na Kristo. Kwa neema ya Mungu ninyi mmeokolewa. 6Kwa kuungana na Kristo Yesu, Mungu alitufufua pamoja naye, tukatawale pamoja naye mbinguni. 7Ndivyo alivyopenda kuonyesha kwa watu wa nyakati za baadaye, ukuu wa neema yake aliyotujalia kwa ukarimu katika kuungana kwetu na Kristo Yesu. 8Maana, kwa neema ya Mungu mmekombolewa kwa njia ya imani. Jambo hili si matokeo ya juhudi zenu, bali ni zawadi ya Mungu. 9Wala halitokani na matendo yenu wenyewe, asije mtu akajivunia kitu. 10Sisi ni viumbe vyake Mungu, na kwa kuungana na Kristo Yesu, alituumba kwa ajili ya kuishi maisha ya matendo mema aliyotutayarishia tuyatende.

11Ninyi mlio kwa asili watu wa mataifa mengine--mnaoitwa, "wasiotahiriwa" na Wayahudi ambao hujiita, "Waliotahiriwa," (kwa sababu ya kile wanachoifanyia miili yao) --kumbukeni mlivyokuwa zamani. 12Wakati ule ninyi mlikuwa bila Kristo; mlikuwa nje ya jamii ya Israeli; mlikuwa wageni na hamkuwa na sehemu yoyote katika lile agano la zile ahadi. Mlikuwa bila matumaini Mungu hapa duniani. 13Lakini sasa, kwa kuungana na Kristo Yesu, ninyi ambao hapo awali mlikuwa mbali, mmekaribishwa kwa njia ya damu yake Kristo. 14Maana Kristo mwenyewe ametuletea amani kwa kuwafanya Wayahudi na watu wa mataifa mengine kuwa jamii moja. Kwa mwili wake yeye mwenyewe aliubomoa ule ukuta uliowatenganisha na kuwafanya maadui. 15Aliiondoa ile Sheria ya Wayahudi pamoja na amri zake na kanuni zake, ili kutokana na jamii hizo mbili aumbe jamii moja mpya katika umoja naye na hivyo kuleta amani. 16Kwa mwili wake, Kristo aliuangamiza uadui wao; kwa msalaba wake aliziunganisha jamii hizo kuwa moja na kuzipatanisha na Mungu. 17Basi, Kristo alikuja akahubiri Habari Njema ya amani kwenu ninyi watu wa mataifa mengine mliokuwa mbali na Mungu, na pia kwa Wayahudi ambao walikuwa karibu na Mungu. 18Hivyo, kwa njia yake, sisi sote, Wayahudi na watu wa mataifa mengine, tunaweza kumwendea Baba katika Roho mmoja. 19Basi, ninyi si wageni tena, wala si watu wa nje; ninyi ni raia pamoja na watu wa Mungu, na ni watu wa jamaa ya Mungu. 20Mmejengwa juu ya msingi uliowekwa na mitume na manabii, naye Kristo mwenyewe ndiye jiwe kuu la msingi. 21Yeye ndiye mwenye kulitengeneza jengo lote na kulikuza hata liwe hekalu takatifu kwa ajili ya B wana. 22Katika kuungana naye, ninyi pia mnajengwa pamoja na wote wengine, muwe makao ya Mungu kwa njia ya Roho wake.



Public Domain Swahili New Testament -- PLEASE MAKE COPIES FOR YOUR FRIENDS, NO ROYALTY DUE.

Bible Hub

Ephesians 1
Top of Page
Top of Page