Marko 5
Swahili NT
1Basi, wakafika katika nchi ya Wagerase, ng'ambo ya ziwa. 2Mara tu Yesu aliposhuka mashuani, mtu mmoja aliyepagawa na pepo mchafu alitoka makaburini, akakutana naye. 3Mtu huyo alikuwa akiishi makaburini wala hakuna mtu aliyeweza tena kumfunga kwa minyororo. 4Mara nyingi walimfunga kwa pingu na minyororo lakini kila mara aliweza kuikata hiyo minyororo na kuzivunja hizo pingu, wala hakuna mtu aliyeweza kumzuia. 5Mchana na usiku alikaa makaburini na milimani akipaaza sauti na kujikatakata kwa mawe. 6Alipomwona Yesu kwa mbali, alimkimbilia, akamwinamia 7akisema kwa sauti kubwa, "Una shauri gani nami, wewe Yesu Mwana wa Mungu aliye juu? Kwa jina la Mungu, nakusihi usinitese!" 8(Alisema hivyo kwa kuwa Yesu alikuwa amemwambia, "Pepo mchafu, mtoke mtu huyu.") 9Basi, Yesu akamwuliza, "Jina lako nani?" Naye akajibu, "Jina langu ni Jeshi, maana sisi tu wengi." 10Kisha akamsihi Yesu asiwafukuze hao pepo katika nchi ile. 11Kulikuwa na kundi kubwa la nguruwe malishoni kwenye mteremko wa mlima. 12Basi, hao pepo wakamsihi, "Utupeleke kwa hao nguruwe, tuwaingie." 13Naye akawaruhusu. Basi, hao pepo wachafu wakatoka, wakawaingia wale nguruwe. Kundi lote la nguruwe wapatao elfu mbili likaporomoka kwenye ule mteremko mkali mpaka ziwani, likatumbukia majini.

14Wachungaji wa hao nguruwe walikimbia, wakatangaza jambo hilo mjini na mashambani. Watu wakafika kuona yaliyotukia. 15Wakamwendea Yesu, wakamwona na mtu yuleyule aliyekuwa amepagawa na jeshi la pepo ameketi chini, amevaa nguo na ana akili yake sawa, wakaogopa. 16Watu walishuhudia tukio hilo wakaeleza wengine mambo yaliyompata huyo mtu aliyekuwa amepagawa na pepo na juu ya wale nguruwe. 17Basi, wakaanza kumwomba aondoke katika nchi yao. 18Yesu alipokuwa anapanda mashuani, yule mtu aliyekuwa amepagawa na pepo akamwomba amruhusu kwenda naye. 19Lakini Yesu akamkatalia. Badala yake akamwambia, "Nenda nyumbani kwa jamaa yako, ukawaambie mambo yote Bwana aliyokutendea na jinsi alivyokuonea huruma." 20Basi, huyo mtu akaenda, akaanza kutangaza huko Dekapoli mambo yote Yesu aliyomtendea; watu wote wakashangaa.

21Yesu alivukia tena upande wa pili wa ziwa kwa mashua. Umati mkubwa wa watu ukakusanyika mbele yake, naye akawa amesimama kando ya ziwa. 22Hapo akaja mmojawapo wa maofisa wa sunagogi, jina lake Yairo. Alipomwona Yesu, akajitupa mbele ya miguu yake, 23akamsihi akisema, "Binti yangu mdogo ni mgonjwa karibu kufa. Twende tafadhali, ukamwekee mikono yako, apate kupona na kuishi." 24Basi, Yesu akaondoka pamoja naye. Watu wengi sana wakamfuata, wakawa wanamsonga kila upande.

25Mmojawapo alikuwa mwanamke mwenye ugonjwa wa kutokwa damu kwa muda wa miaka kumi na miwili. 26Mwanamke huyo alikuwa amekwisha sumbuka sana kuwaendea waganga wengi. Na ingawa alikuwa amekwisha tumia mali yake yote, hakupata nafuu bali hali yake ilizidi kuwa mbaya. 27Alikuwa amesikia habari za Yesu, na hivyo akaupenya msongamano wa watu kutoka nyuma, akagusa vazi lake. 28Alifanya hivyo, maana alijisemea, "Nikigusa tu vazi lake, nitapona." 29Mara chemchemi ya damu yake ikakauka, akajisikia mwilini mwake kwamba ameponywa ugonjwa wake. 30Yesu alitambua mara kwamba nguvu imemtoka. Basi akaugeukia ule umati wa watu, akauliza, "Nani aliyegusa mavazi yangu?" 31Wanafunzi wake wakamjibu, "Unaona jinsi watu wanavyokusonga; mbona wauliza nani aliyekugusa?" 32Lakini Yesu akaendelea kutazama amwone huyo aliyefanya hivyo. 33Hapo huyo mwanamke, akifahamu yaliyompata, akajitokeza akitetemeka kwa hofu, akajitupa chini mbele ya Yesu na kusema ukweli wote. 34Yesu akamwambia, "Binti, imani yako imekuponya. Nenda kwa amani, upone kabisa ugonjwa wako."

35Yesu alipokuwa bado anaongea, watu walifika kutoka nyumbani kwa yule ofisa wa sunagogi, wakamwambia, "Binti yako amekwisha kufa. Ya nini kuendelea kumsumbua Mwalimu?" 36Lakini, bila kujali walichosema, Yesu akamwambia mkuu wa sunagogi, "Usiogope, amini tu." 37Wala hakumruhusu mtu yeyote kufuatana naye ila Petro, Yakobo na Yohane nduguye Yakobo. 38Wakafika nyumbani kwa ofisa wa sunagogi naye Yesu akasikia makelele, kilio na maombolezo mengi. 39Akaingia ndani, akawaambia, "Mbona mnapiga kelele na kulia? Msichana hakufa, amelala tu." 40Lakini wao wakamcheka. Basi, akawaondoa wote nje, akawachukua baba na mama ya huyo msichana na wale wanafunzi wake, wakaingia chumbani alimokuwa huyo msichana. 41Kisha akamshika mkono, akamwambia, "Talitha, kumi," maana yake, "Msichana, nakwambia, amka!" 42Mara msichana akasimama, akaanza kutembea. (Alikuwa na umri wa miaka kumi na miwili.) Hapo watu wakashangaa kupita kiasi. 43Yesu akawakataza sana wasimjulishe mtu jambo hilo. Kisha akawaambia wampe huyo msichana chakula.



Public Domain Swahili New Testament -- PLEASE MAKE COPIES FOR YOUR FRIENDS, NO ROYALTY DUE.

Bible Hub

Mark 4
Top of Page
Top of Page