Matendo Ya Mitume 26
Swahili NT
1Basi, Agripa akamwambia Paulo, "Unaruhusiwa kujitetea." Hapo Paulo alinyosha mkono wake akajitetea hivi:

2Mfalme Agripa, ninajiona mwenye bahati leo kujitetea mbele yako kuhusu yale mashtaka yote ambayo Wayahudi walikuwa wamesema juu yangu. 3Hasa kwa vile wewe mwenyewe ni mtaalamu wa desturi za Wayahudi na migogoro yao, ninakuomba basi unisikilize kwa uvumilivu.

4Wayahudi wanajua habari za maisha yangu tangu utoto, jinsi nilivyoishi tangu mwanzo kati ya taifa langu huko Yerusalemu. 5Wananifahamu kwa muda mrefu, na wanaweza kushuhudia, kama wakipenda, kwamba tangu mwanzo niliishi kama mmoja wa kikundi chenye siasa kali zaidi katika dini yetu, yaani kikundi cha Mafarisayo. 6Na sasa niko hapa nihukumiwe kwa sababu ninaitumainia ile ahadi ambayo Mungu aliwaahidia babu zetu. 7Ahadi hiyo ndiyo ileile inayotumainiwa na makabila kumi na mawili ya taifa letu, wakimtumikia Mungu kwa dhati mchana na usiku. Mheshimiwa mfalme, Wayahudi wananishtaki kwa sababu ya tumaini hilo! 8Kwa nini ninyi mnaona shida sana kuamini kwamba Mungu huwafufua wafu?

9Kwa kweli mimi mwenyewe niliamini kwamba ni wajibu wangu kufanya mambo mengi kulipinga jina la Yesu wa Nazareti. 10Mambo hayo ndiyo niliyoyafanya huko Yerusalemu. Mimi binafsi, nikiwa nimepewa mamlaka kutoka kwa makuhani wakuu, nilipata kuwatia gerezani wengi wa watu wa Mungu. Nao walipohukumiwa kuuawa, nilipiga kura ya kukubali. 11Mara nyingi niliwafanya waadhibiwe katika masunagogi yote nikiwashurutisha waikane imani yao. Hasira yangu kwao ilikuwa kubwa hata nikawasaka mpaka miji ya mbali.

12Kwa mujibu huohuo, nilikwenda Damasko wakati mmoja, nikiwa na mamlaka na maagizo kutoka kwa makuhani wakuu. 13Mheshimiwa, wakati nilipokuwa njiani, saa sita mchana, niliona mwanga mkubwa kuliko wa jua ukiangaza kutoka mbinguni, ukanizunguka mimi na wale wasafiri wenzangu. 14Sisi sote tulianguka chini, nami nikasikia sauti ikiniambia kwa Kiebrania: Saulo, Saulo! Kwa nini unanitesa? Unajiumiza bure kama punda anayepiga teke fimbo ya bwana wake. 15Mimi nikauliza: Ni nani wewe Bwana? Naye Bwana akajibu: Mimi ni Yesu ambaye wewe unamtesa. 16Haidhuru, inuka sasa; simama wima. Nimekutokea ili nikuweke rasmi kuwa mtumishi wangu. Utawathibitishia watu wengine mambo uliyoyaona leo na yale ambayo bado nitakuonyesha. 17Nitakuokoa na watu wa Israeli na watu wa mataifa mengine ambao mimi ninakutuma kwao. 18Utayafumbua macho yao na kuwawezesha watoke gizani na kuingia katika mwanga; watoke katika utawala wa Shetani, wamgeukie Mungu; ili kwa kuamini, wapate kusamehewa dhambi na kuchukua nafasi yao kati ya wale ambao wamepata kuwa watu wa Mungu.

19Hivyo, mfalme Agripa, sikuweza kuwa mkaidi kwa maono hilo la mbinguni. 20Ila nilianza kuhubiri kwanza kwa watu wa Damasko, halafu kwa wale wa Yerusalemu na nchi yote ya Yudea, na pia kwa watu wa mataifa mengine. Niliwahimiza wamgeukie Mungu na kuonyesha kwa vitendo kwamba wamebadilisha mioyo yao. 21Kwa sababu hiyo, Wayahudi walinikamata nikiwa Hekaluni, wakajaribu kuniua. 22Lakini Mungu alinisaidia; na hivyo mpaka siku ya leo nimesimama imara nikitoa ushuhuda kwa wote, wakubwa na wadogo. Ninayosema ni yale ambayo manabii na Mose walisema yatatukia; 23yaani ilimpasa Kristo ateseke na kuwa wa kwanza kufufuka kutoka wafu, ili atangaze kwamba mwanga wa ukombozi unawaangazia sasa watu wote, Wayahudi na pia watu wa mataifa mengine."

24Paulo alipofika hapa katika kujitetea kwake, Festo alisema kwa sauti kubwa, "Paulo! Una wazimu! Kusoma kwako kwingi kunakutia wazimu!" 25Lakini Paulo akasema, "Sina wazimu mheshimiwa Festo: Ninachosema ni ukweli mtupu. 26Wewe Mfalme unayafahamu mambo haya, kwa hiyo ninaweza kuongea bila uoga mbele yako. Sina mashaka kwamba matukio hayo yanajulikana kwako maana jambo hili halikutendeka mafichoni. 27Mfalme Agripa, je, una imani na manabii? Najua kwamba unaamini." 28Agripa akamjibu Paulo, "Kidogo tu utanifanya Mkristo!" 29Paulo akamjibu, "Namwomba Mungu kwamba, kwa muda mfupi au mrefu, si wewe tu bali wote wanaonisikia leo wapate kuwa kama nilivyo mimi, lakini bila hii minyororo."

30Hapo mfalme Agripa, mkuu wa mkoa, Bernike na wale wote waliokuwa pamoja nao, walisimama. 31Walipokwisha ondoka, waliambiana, "Mtu huyu hakufanya chochote kinachostahili adhabu ya kifo au kifungo." 32Naye Agripa akamwambia Festo, "Mtu huyu angeweza kufunguliwa kama asingalikuwa amekata rufani kwa Kaisari."Public Domain Swahili New Testament -- PLEASE MAKE COPIES FOR YOUR FRIENDS, NO ROYALTY DUE.

Bible Hub

Acts 25
Top of Page
Top of Page