Marko 7
Swahili NT
1Baadhi ya Mafarisayo na walimu wa Sheria waliokuwa wametoka Yerusalemu walikusanyika mbele ya Yesu. 2Waliona kwamba baadhi ya wanafunzi wake walikula mikate kwa mikono najisi, yaani bila kunawa. 3Maana Mafarisayo na Wayahudi wengine wote huzingatia mapokeo ya wazee wao: hawali kitu kabla ya kunawa mikono ipasavyo. 4Tena hawali kitu chochote kutoka sokoni mpaka wamekiosha kwanza. Kuna pia desturi nyingine walizopokea kama vile namna ya kuosha vikombe, sufuria na vyombo vya shaba. 5Basi, Mafarisayo na walimu wa Sheria wakamwuliza Yesu, "Mbona wanafunzi wako hawayajali mapokeo tuliyopokea kwa wazee wetu, bali hula chakula kwa mikono najisi?"

6Yesu akawajibu, "Wanafiki ninyi! Nabii Isaya alitabiri ukweli juu yenu alipoandika: Watu hawa, asema Mungu, huniheshimu kwa maneno matupu, lakini mioyoni mwao wako mbali nami.

7Kuniabudu kwao hakufai, maana mambo wanayofundisha ni maagizo ya kibinadamu tu.

8Ninyi mnaiacha amri ya Mungu na kushikilia maagizo ya watu."

9Yesu akaendelea kusema, "Ninyi mnajua kuepa kwa ujanja sheria ya Mungu kwa ajili ya kufuata mapokeo yenu. 10Maana Mose aliamuru: Waheshimu baba yako na mama yako, na, Anayemlaani baba au mama, lazima afe. 11Lakini ninyi mwafundisha, Kama mtu anacho kitu ambacho angeweza kuwasaidia nacho baba au mama yake, lakini akasema kwamba kitu hicho ni Korbani (yaani ni zawadi kwa Mungu), 12basi, halazimiki tena kuwasaidia wazazi wake. 13Hivyo ndivyo mnavyodharau neno la Mungu kwa ajili ya mafundisho mnayopokezana. Tena mnafanya mambo mengi ya namna hiyo."

14Yesu aliuita tena ule umati wa watu, akawaambia, "Nisikilizeni nyote, mkaelewe. 15Hakuna kitu kinachoingia ndani ya mtu toka nje ambacho chaweza kumtia mtu najisi. Lakini kinachotoka ndani ya mtu ndicho kinachomtia mtu najisi." 16Mwenye masikio na asikie!

17Alipouacha umati wa watu na kuingia nyumbani, wanafunzi wake walimwuliza maana ya huo mfano. 18Naye akawaambia, "Je, hata ninyi hamwelewi? Je, hamwelewi kwamba kitu kinachomwingia mtu toka nje hakiwezi kumtia unajisi, 19kwa maana hakimwingii moyoni, ila tumboni, na baadaye hutolewa nje chooni?" (Kwa kusema hivyo, Yesu alivihalalisha vyakula vyote.) 20Akaendelea kusema, "Kinachotoka ndani ya mtu ndicho kinachomtia najisi. 21Kwa maana kutoka ndani, katika moyo wa mtu, hutoka mawazo mabaya, uasherati, wizi, uuaji, 22uzinzi, uchoyo, uovu, udanganyifu, ufisadi, wivu, kashfa, kiburi na upumbavu. 23Maovu hayo yote yatoka ndani ya mtu, nayo humtia mtu najisi."

24Yesu aliondoka hapo, akaenda hadi wilaya ya Tiro. Huko aliingia katika nyumba moja na hakutaka mtu ajue; lakini hakuweza kujificha. 25Mwanamke mmoja ambaye binti yake alikuwa na pepo, alisikia habari za Yesu. Basi, akaja akajitupa chini mbele ya miguu yake. 26Mama huyo alikuwa Mgiriki, mwenyeji wa Sirofoinike. Basi, akamwomba Yesu amtoe binti yake pepo mchafu. 27Yesu akamwambia, "Kwanza watoto washibe; kwa maana si vizuri kuchukua chakula cha watoto na kuwatupia mbwa." 28Lakini huyo mama akasema, "Sawa, Bwana, lakini hata mbwa walio chini ya meza hula makombo ya watoto." 29Yesu akamwambia, "Kwa sababu ya neno hilo, nenda. Pepo amemtoka binti yako!" 30Basi, akaenda nyumbani kwake, akamkuta mtoto amelala kitandani, na pepo amekwisha mtoka.

31Kisha Yesu aliondoka wilayani Tiro, akapitia Sidoni, akafika ziwa Galilaya kwa kupitia nchi ya Dekapoli. 32Basi, wakamletea bubu-kiziwi, wakamwomba amwekee mikono. 33Yesu akamtenga na umati wa watu, akamtia vidole masikioni, akatema mate na kumgusa ulimi. 34Kisha akatazama juu mbinguni, akapiga kite, akamwambia, "Efatha," maana yake, "Funguka." 35Mara masikio yake yakafunguka na ulimi wake ukafunguliwa, akaanza kusema sawasawa. 36Yesu akawaamuru wasimwambie mtu juu ya jambo hilo. Lakini kadiri alivyowakataza, ndivyo walivyozidi kutangaza habari hiyo. 37Watu walishangaa sana, wakasema, "Amefanya yote vyema: amewajalia viziwi kusikia, na bubu kusema!"



Public Domain Swahili New Testament -- PLEASE MAKE COPIES FOR YOUR FRIENDS, NO ROYALTY DUE.

Bible Hub

Mark 6
Top of Page
Top of Page