Matayo 1
Swahili NT
1Yesu Kristo alikuwa mzawa wa Daudi, mzawa wa Abrahamu. Hii ndiyo orodha ya ukoo wake:

2Abrahamu alimzaa Isaka, Isaka alimzaa Yakobo, Yakobo alimzaa Yuda na ndugu zake, 3Yuda alimzaa Faresi na Zera (mama yao alikuwa Tamari), Faresi alimzaa Hesroni, Hesroni alimzaa Rami, 4Rami alimzaa Aminadabu, Aminadabu alimzaa Nashoni, Nashoni alimzaa Salmoni, 5Salmoni alimzaa Boazi (mama yake Boazi alikuwa Rahabu). Boazi na Ruthi walikuwa wazazi wa Obedi, Obedi alimzaa Yese, 6naye Yese alimzaa Mfalme Daudi. Daudi alimzaa Solomoni (mama yake Solomoni alikuwa mke wa Uria). 7Solomoni alimzaa Rehoboamu, Rehoboamu alimzaa Abiya, Abiya alimzaa Asa, 8Asa alimzaa Yehoshafati, Yehoshafati alimzaa Yoramu, Yoramu alimzaa Uzia, 9Uzia alimzaa Yothamu, Yothamu alimzaa Ahazi, Ahazi alimzaa Hezekia, 10Hezekia alimzaa Manase, Manase alimzaa Amoni, Amoni alimzaa Yosia, 11Yosia alimzaa Yekonia na ndugu zake. Huo ulikuwa wakati Wayahudi walipopelekwa uhamishoni Babuloni.

12Baada ya Wayahudi kupelekwa uhamishomi Babuloni: Yekonia alimzaa Shealtieli, Shealtieli alimzaa Zerobabeli, 13Zerobabeli alimzaa Abiudi, Abiudi alimzaa Eliakimu, Eliakimu alimzaa Azori, 14Azori alimzaa Zadoki, Zadoki alimzaa Akimu, Akimu alimzaa Eliudi, 15Eliudi alimzaa Eleazeri, Eleazeri alimzaa Mathani, Mathani alimzaa Yakobo, 16Yakobo alimzaa Yosefu, aliyekuwa mume wake Maria, mama yake Yesu, aitwaye Kristo.

17Basi, kulikuwa na vizazi kumi na vinne tangu Abrahamu mpaka Daudi, vizazi kumi na vinne tangu Daudi mpaka Wayahudi walipochukuliwa mateka Babuloni, na vizazi kumi na vinne tangu kuchukuliwa mateka mpaka wakati wa Kristo.

18Basi, hivi ndivyo Yesu Kristo alivyozaliwa: Maria, mama yake, alikuwa ameposwa na Yosefu. Lakini kabla hawajakaa pamoja kama mume na mke, alionekana kuwa mja mzito kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. 19Yosefu, mumewe, kwa vile alikuwa mwadilifu, hakutaka kumwaibisha hadharani; hivyo alikusudia kumwacha kwa siri. 20Alipokuwa bado anawaza jambo hilo, malaika wa Bwana alimtokea katika ndoto, akamwambia, "Yosefu, mwana wa Daudi, usiogope kumchukua Maria awe mke wako, maana amekuwa mja mzito kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. 21Atajifungua mtoto wa kiume, nawe utampa jina Yesu, kwa kuwa yeye atawaokoa watu wake kutoka katika dhambi zao." 22Basi, haya yote yalitukia ili litimie lile neno Bwana alilosema kwa njia ya nabii: 23Bikira atachukua mimba, atamzaa mtoto wa kiume, naye ataitwa Emanueli (maana yake, "Mungu yu pamoja nasi"). 24Hivyo, Yosefu alipoamka usingizini alifanya kama malaika huyo alivyomwambia, akamchukua mke wake nyumbani. 25Lakini hakumjua kamwe kimwili hata Maria alipojifungua mtoto wa kiume. Naye Yosefu akampa jina Yesu.



Public Domain Swahili New Testament -- PLEASE MAKE COPIES FOR YOUR FRIENDS, NO ROYALTY DUE.

Bible Hub

Malachi 4
Top of Page
Top of Page