Luka 12
Swahili NT
1Wakati watu kwa maelfu walipokuwa wamekusanyika hata wakawa wanakanyagana, Yesu aliwaambia kwanza wanafunzi wake, "Jihadharini na chachu ya Mafarisayo, yaani unafiki. 2Kila kilichofunikwa kitafunuliwa, kila kilichofichika kitafichuliwa. 3Kwa hiyo, kila mliyosema gizani, watu watayasikia katika mwanga, na kila mliyonong'ona faraghani milango imefungwa, yatatangazwa juu ya nyumba.

4Nawaambieni ninyi rafiki zangu: msiwaogope wale wanaoua mwili, wasiweze kufanya kitu kingine zaidi. 5Nitawaonyesheni yule ambaye ni lazima kumwogopa: mwogopeni yule ambaye baada ya kuua ana uwezo wa kumtupa mtu katika moto wa Jehanamu. Naam, ninawaambieni, mwogopeni huyo. 6Inajulikana kwamba shomoro watano huuzwa kwa senti kumi, au sivyo? Lakini mbele ya Mungu hasahauliki hata mmoja. 7Lakini hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote. Msiogope, basi, ninyi mna thamani zaidi kuliko shomoro wengi!

8Nawaambieni kweli, kila mtu anayekiri hadharani kwamba yeye ni wangu, Mwana wa Mtu naye atakiri mbele ya malaika wa Mungu kwamba mtu huyo ni wake. 9Lakini, mtu yeyote anayenikana mbele ya watu, naye atakanwa mbele ya malaika wa Mungu. 10Yeyote anayesema neno la kumpinga Mwana wa Mtu atasamehewa; lakini anayemkufuru Roho Mtakatifu hatasamehewa. 11Watakapowapeleka ninyi mbele ya masunagogi na mbele ya wakuu na watawala msiwe na wasiwasi juu ya jinsi mtakavyojitetea au jinsi mtakavyosema. 12Kwa maana wakati huo Roho Mtakatifu atawafundisheni kile mnachopaswa kusema."

13Mtu mmoja katika ule umati wa watu akamwambia, "Mwalimu, mwambie ndugu yangu tugawane urithi aliotuachia baba." 14Yesu akamjibu, "Rafiki, ni nani aliyeniweka mimi mwamuzi au msuluhishi kati yenu?" 15Basi, akawaambia wote, "Jihadharini na kila aina ya tamaa; maana uzima wa mtu hautegemei wingi wa vitu alivyo navyo." 16Kisha akawaambia mfano: "Kulikuwa na tajiri mmoja ambaye shamba lake lilizaa mavuno mengi. 17Tajiri huyo akafikiri moyoni mwake: Nitafanyaje nami sina mahali pa kuhifadhia mavuno yangu? 18Nitafanya hivi: nitabomoa ghala zangu na kujenga kubwa zaidi, na humo nitahifadhi mavuno yangu yote na mali yangu. 19Hapo nitaweza kuiambia roho yangu: sasa unayo akiba ya matumizi kwa miaka na miaka. Ponda mali, ule, unywe na kufurahi. 20Lakini Mungu akamwambia: Mpumbavu wewe; leo usiku roho yako itachukuliwa. Na vitu vile vyote ulivyojilundikia vitakuwa vya nani?" 21Yesu akamaliza kwa kusema "Ndivyo ilivyo kwa mtu anayejilundikia mali kwa ajili yake mwenyewe, lakini si tajiri mbele ya Mungu."

22Kisha Yesu akawaambia wanafunzi wake, "Kwa sababu hiyo nawaambieni, msiwe na wasiwasi juu ya chakula mnachohitaji ili kuishi, wala juu ya mavazi mnayohitaji kwa ajili ya miili yenu. 23Kwa sababu uzima ni bora kuliko chakula, na mwili ni bora kuliko mavazi. 24Chukueni kwa mfano, kunguru: hawapandi, hawavuni wala hawana ghala yoyote. Hata hivyo, Mungu huwalisha. Ninyi mna thamani zaidi kuliko ndege! 25Ni nani kati yenu kwa kuwa na wasiwasi anaweza kuongeza urefu wa maisha yake? 26Basi, kama hamwezi kufanya jambo dogo kama hilo, kwa nini kuwa na wasiwasi juu ya yale mengine? 27Angalieni maua jinsi yanavyomea. Hayafanyi kazi wala hayafumi. Hata hivyo, nawahakikishieni kwamba hata Solomoni mwenyewe na fahari zake zote hakupata kuvikwa vizuri kama ua mojawapo. 28Lakini, kama Mungu hulivika vizuri jani la shambani ambalo leo liko na kesho latupwa motoni, je, hatawafanyia ninyi zaidi? Enyi watu wenye imani haba! 29Basi, msivurugike akili, mkihangaika daima juu ya mtakachokula au mtakachokunywa. 30Kwa maana hayo yote ndiyo yanayohangaikiwa na watu wasiomjua Mungu. Baba yenu anajua kwamba mnahitaji vitu hivyo. 31Shughulikieni kwanza Ufalme wa Mungu, na hayo yote mtapewa kwa ziada. 32Msiogope, enyi kundi dogo! Maana Baba yenu amependa kuwapeni Ufalme.

33Uzeni mali yenu mkawape maskini misaada. Jifanyieni mifuko isiyochakaa, na jiwekeeni hazina mbinguni ambako haitapungua. Huko wezi hawakaribii, wala nondo hawaharibu. 34Pale ilipo hazina yako, ndipo pia utakapokuwa moyo wako.

35Muwe tayari! Jifungeni mkanda kiunoni, na taa zenu ziwe zinawaka; 36muwe kama watumishi wanaomngojea bwana wao arudi kutoka arusini, ili wamfungulie mara atakapobisha hodi. 37Heri yao watumishi wale ambao bwana wao atakaporudi atawakuta wanakesha! Nawaambieni hakika, huyo bwana atajifunga mkanda kiunoni, atawaketisha mezani na kuwahudumia. 38Heri yao watumishi hao ikiwa bwana wao atawakuta wanakesha hata ikiwa atarudi usiku wa manane au alfajiri.

39Jueni kwamba, kama mwenye nyumba angejua saa ambayo mwizi atakuja, angekesha, wala hangeiacha nyumba yake ivunjwe. 40Nanyi, kadhalika muwe tayari, maana Mwana wa Mtu atakuja saa msiyoitazamia."

41Petro akamwambia, "Bwana, mfano huo ni kwa ajili yetu tu, au ni kwa ajili ya watu wote?" 42Bwana akajibu, "Ni nani basi, mtumishi aliye mwaminifu na mwenye busara, ambaye bwana wake atamweka juu ya watumishi wake ili awape chakula wakati ufaao? 43Heri yake mtumishi huyo ikiwa bwana wake atakaporudi atamkuta akifanya hivyo. 44Hakika atampa madaraka juu ya mali yake yote. 45Lakini, kama mtumishi huyo atafikiri moyoni mwake: na kusema: Bwana wangu amekawia sana kurudi halafu aanze kuwapiga watumishi wenzake, wa kiume au wa kike, na kula, kunywa na kulewa, 46bwana wake atarudi siku asiyoitazamia na saa asiyoijua; atamkatilia mbali na kumweka fungu moja na wasioamini. 47Mtumishi ambaye anajua matakwa ya bwana wake lakini hajiweki tayari kufanya anavyotakiwa, atapigwa sana. 48Lakini yule afanyaye yanayostahili adhabu bila kujua, atapigwa kidogo. Aliyepewa vingi atatakiwa vingi; aliyekabidhiwa vingi zaidi atatakiwa kutoa vingi zaidi.

49Nimekuja kuwasha moto duniani, laiti ungekuwa umewaka tayari! 50Ninao ubatizo ambao inanipasa niupokee; jinsi gani ninavyohangaika mpaka ukamilike! 51Mnadhani nimekuja kuleta amani duniani? Hata kidogo; si amani bali utengano. 52Na tangu sasa, jamaa ya watu watano itagawanyika; watatu dhidi ya wawili, na wawili dhidi ya watatu. 53Baba atakuwa dhidi ya mwanawe, mwana dhidi ya baba yake; mama dhidi ya bintiye, binti dhidi ya mama yake; mama mkwe dhidi ya mke wa mwanawe na huyo dhidi ya mama mkwe wake."

54Yesu akayaambia tena makundi ya watu, "Mnapoona mawingu yakitokea upande wa magharibi, mara mwasema: Mvua itanyesha, na kweli hunyesha. 55Mnapoona upepo wa kusi unavuma, mwasema Kutakuwa na hali ya joto na ndivyo inavyokuwa. 56Enyi wanafiki! Mnajua kutabiri hali ya hewa kwa kuangalia dunia na anga; kwa nini basi, hamwezi kujua maana ya nyakati hizi?

57Na kwa nini hamwezi kujiamulia wenyewe jambo jema la kufanya? 58Maana kama mshtaki wako anakupeleka mahakamani, ingekuwa afadhali kwako kupatana naye mkiwa bado njiani, ili asije akakupeleka mbele ya hakimu, naye hakimu akakutoa kwa polisi, nao wakakutia ndani. 59Hakika hutatoka huko nakwambia, mpaka utakapomaliza kulipa senti ya mwisho."



Public Domain Swahili New Testament -- PLEASE MAKE COPIES FOR YOUR FRIENDS, NO ROYALTY DUE.

Bible Hub

Luke 11
Top of Page
Top of Page