Luka 18
Swahili NT
1Basi, Yesu aliwasimulia mfano kuonyesha kwamba ni lazima kusali daima bila kukata tamaa. 2Alisema: "Katika mji mmoja kulikuwa na hakimu ambaye hakuwa anamcha Mungu wala kumjali binadamu. 3Katika mji huohuo, kulikuwa pia na mama mmoja mjane, ambaye alimwendea huyo hakimu mara nyingi akimwomba amtetee apate haki yake kutoka kwa adui yake. 4Kwa muda mrefu huyo hakimu hakupenda kumtetea huyo mjane; lakini, mwishowe akajisemea: Ingawa mimi simchi Mungu wala simjali binadamu, 5lakini kwa vile huyu mjane ananisumbua, nitamtetea; la sivyo ataendelea kufika hapa, na mwisho atanichosha kabisa!" 6Basi, Bwana akaendelea kusema, "Sikieni jinsi alivyosema huyo hakimu mbaya. 7Je, ndio kusema Mungu hatawatetea wale aliowachagua, ambao wanamlilia mchana na usiku? Je, atakawia kuwasikiliza? 8Nawaambieni atawatetea upesi. Hata hivyo, je, kutakuwako na imani duniani wakati Mwana wa Mtu atakapokuja?"

9Halafu Yesu aliwaambia pia mfano wa wale ambao walijiona kuwa wema na kuwadharau wengine. 10Watu wawili walipanda kwenda Hekaluni kusali: mmoja Mfarisayo, na mwingine mtoza ushuru. 11Huyo Mfarisayo akasimama, akasali kimoyomoyo: Ee Mungu, nakushukuru kwa vile mimi si kama watu wengine: walafi, wadanganyifu au wazinzi. Nakushukuru kwamba mimi si kama huyu mtoza ushuru. 12Nafunga mara mbili kwa juma, natoa zaka sehemu ya kumi ya pato langu. 13Lakini yule mtoza ushuru, akiwa amesimama kwa mbali bila hata kuinua macho yake mbinguni, ila tu akijipiga kifua kwa huzuni, alisema: Ee Mungu, unionee huruma mimi mwenye dhambi. 14Nawaambieni, huyu mtoza ushuru alirudi nyumbani akiwa amesamehewa. Lakini yule mwingine, sivyo. Kwa maana kila anayejikweza atashushwa, na kila anayejishusha atakwezwa."

15Watu walimletea Yesu watoto wadogo ili awawekee mikono yake. Wanafunzi walipowaona, wakawazuia kwa maneno makali. 16Lakini Yesu akawaita kwake akisema: "Waacheni hao watoto waje kwangu, wala msiwazuie, kwa maana Ufalme wa Mungu ni kwa ajili ya watu kama hawa. 17Nawaambieni kweli, mtu yeyote asiyeupokea Ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo, hataingia katika Ufalme huo."

18Kiongozi mmoja, Myahudi, alimwuliza Yesu, "Mwalimu mwema, nifanye nini ili niweze kuupata uzima wa milele?" 19Yesu akamwambia, "Mbona waniita mwema? Hakuna aliye mwema ila Mungu peke yake. 20Unazijua amri: Usizini; usiue; usiibe; usitoe ushahidi wa uongo; waheshimu baba yako na mama yako." 21Yeye akasema, "Hayo yote nimeyazingatia tangu ujana wangu." 22Yesu aliposikia hayo akamwambia, "Unatakiwa bado kufanya kitu kimoja: uza kila ulicho nacho, wagawie maskini, na hivyo utakuwa na hazina yako mbinguni; halafu njoo unifuate." 23Lakini huyo mtu aliposikia hayo, alihuzunika sana kwa sababu alikuwa tajiri sana. 24Yesu alipoona akihuzunika hivyo, akasema, "Jinsi gani ilivyo vigumu kwa matajiri kuingia katika Ufalme wa Mungu! 25Naam, ni rahisi zaidi kwa ngamia kupita katika tundu la sindano, kuliko tajiri kuingia katika Ufalme wa Mungu." 26Wale watu waliposikia hayo, wakasema, "Nani basi, atakayeokolewa?" 27Yesu akajibu, "Yasiyowezekana kwa binadamu, yanawezekana kwa Mungu."

28Naye Petro akamwuliza, "Na sisi je? Tumeacha vitu vyote tukakufuata!" 29Yesu akawaambia, "Kweli nawaambieni, mtu yeyote aliyeacha nyumba au mke au kaka au wazazi au watoto kwa ajili ya Ufalme wa Mungu, 30atapokea mengi zaidi wakati huu wa sasa, na kupokea uzima wa milele wakati ujao."

31Yesu aliwachukua kando wale kumi na wawili, akawaambia, "Sikilizeni! Tunakwenda Yerusalemu na huko kila kitu kilichoandikwa na manabii kuhusu Mwana wa Mtu kitakamilishwa. 32Kwa maana atakabidhiwa kwa watu wa mataifa nao watamtendea vibaya na kumtemea mate. 33Watampiga mijeledi, watamuua; lakini siku ya tatu atafufuka." 34Lakini wao hawakuelewa hata kidogo jambo hilo; walikuwa wamefichwa maana ya maneno hayo, na hawakutambua yaliyosemwa.

35Wakati Yesu alipokaribia Yeriko, kulikuwa na mtu mmoja kipofu ameketi njiani akiomba. 36Aliposikia umati wa watu ukipita aliuliza, "Kuna nini?" 37Wakamwambia, "Yesu wa Nazareti anapita." 38Naye akapaza sauti akisema, "Yesu, Mwana wa Daudi, nihurumie!" 39Wale watu waliotangulia wakamkemea wakimwambia anyamaze; lakini yeye akazidi kupaza sauti: "Mwana wa Daudi, nihurumie;" 40Yesu alisimama, akaamuru wamlete mbele yake. Yule kipofu alipofika karibu, Yesu akamwuliza, 41Unataka nikufanyie nini? Naye akamjibu, "Bwana, naomba nipate kuona tena." 42Yesu akamwambia, "Ona! Imani yako imekuponya." 43Na mara yule aliyekuwa kipofu akapata kuona, akamfuata Yesu akimtukuza Mungu. Watu wote walipoona hayo, wakamsifu Mungu.



Public Domain Swahili New Testament -- PLEASE MAKE COPIES FOR YOUR FRIENDS, NO ROYALTY DUE.

Bible Hub

Luke 17
Top of Page
Top of Page