Matendo Ya Mitume 13
Swahili NT
1Katika kanisa la Antiokia kulikuwa na watu wengine waliokuwa manabii na walimu; miongoni mwao akiwa Barnaba, Simoni aitwaye pia Mweusi, Lukio wa Kurene, Manaeni ambaye alikuwa amelelewa pamoja na mfalme Herode, na Saulo. 2Walipokuwa wanafanya ibada yao kwa Bwana na kufunga, Roho Mtakatifu alisema: "Niteulieni Barnaba na Saulo kwa ajili ya kazi niliyowaitia." 3Basi, baada ya kusali na kufunga zaidi, wakawawekea mikono, wakawaacha waende zao.

4Basi, Barnaba na Saulo walipokwisha tumwa na Roho Mtakatifu, walishuka hadi Seleukia, na kutoka huko walipanda meli hadi kisiwa cha Kupro. 5Walipofika Salami walihubiri neno la Mungu katika masunagogi ya Kiyahudi. Yohane (Marko) alikuwa msaidizi wao. 6Walitembea toka upande mmoja wa kisiwa mpaka Pafo upande wa pili, na huko walimkuta mchawi mmoja Myahudi aitwaye Baryesu ambaye alijisingizia kuwa nabii. 7Huyu alikuwa pamoja na Sergio Paulo, mkuu wa kile kisiwa, ambaye alikuwa mtu mwelewa sana. Sergio Paulo aliwaita Barnaba na Saulo ili asikie neno la Mungu. 8Lakini huyo mchawi Elima (kama alivyokuwa anaitwa kwa Kigiriki), alijaribu kuwapinga ili kumzuia huyo mkuu wa kisiwa asije akaigeukia imani ya Kikristo. 9Basi, Saulo ambaye aliitwa pia Paulo, akiwa amejaa Roho Mtakatifu, alimkodolea macho huyo mchawi, 10akasema, "Mdanganyifu wa kupindukia na mlaghai wewe! Wewe ni mtoto wa Ibilisi! Wewe ni adui wa chochote kile kilicho cha kweli; hukomi hata mara moja kujaribu kuzipotosha njia za Bwana zilizonyoka. 11Sasa, mkono wa Bwana utakuadhibu: utakuwa kipofu na hutaweza kuuona mwanga wa jua kwa kitambo." Mara kila kitu kikawa kama ukungu na giza kwake, akaanza kwenda huku na huku akitafuta mtu wa kumshika mkono amwongoze. 12Yule mkuu wa kisiwa alipoona hayo, aliongoka akawa muumini; akastaajabia sana mafundisho aliyosikia juu ya Bwana.

13Kutoka Pafo, Paulo na wenzake walipanda meli wakaenda hadi Perga katika Pamfulia; lakini Yohane (Marko) aliwaacha, akarudi Yerusalemu. 14Lakini wao waliendelea na safari toka Pisga hadi mjini Antiokia Pisidia. Siku ya Sabato waliingia ndani ya Sunagogi, wakakaa. 15Baada ya masomo katika kitabu cha Sheria ya Mose na katika maandiko ya manabii, wakuu wa lile sunagogi waliwapelekea ujumbe huu: "Ndugu, kama mnalo jambo la kuwaambia watu ili kuwapa moyo, semeni." 16Basi, Paulo alisimama, akatoa ishara kwa mkono, akaanza kuongea: "Wananchi wa Israeli na wengine wote mnaomcha Mungu, sikilizeni! 17Mungu wa taifa hili la Israeli aliwateua babu zetu na kuwafanya wawe taifa kubwa walipokuwa ugenini kule Misri. Mungu aliwatoa huko kwa uwezo wake mkuu. 18Aliwavumilia kwa muda wa miaka arobaini kule jangwani. 19Aliyaangamiza mataifa ya nchi ya Kanaani akawapa hao watu wake ile nchi kuwa mali yao. 20Miaka mia nne na hamsini ilipita, halafu akawapatia waamuzi wawaongoze mpaka wakati wa nabii Samweli. 21Hapo wakapendelea kuwa na mfalme, na Mungu akawapa Saulo, mtoto wa Kishi wa kabila la Benyamini, awe mfalme wao kwa muda wa miaka arobaini. 22Baada ya kumwondoa Saulo, Mungu alimteua Daudi kuwa mfalme wao. Mungu alionyesha kibali chake kwake akisema: Nimemwona Daudi mtoto wa Yese; ni mtu anayepatana na moyo wangu; mtu ambaye atatimiza yale yote ninayotaka kuyatenda. 23Kutokana na ukoo wake mtu huyu, Mungu, kama alivyoahidi, amewapelekea watu wa Israeli Mwokozi, ndiye Yesu. 24Kabla ya kuja kwake Yesu, Yohane alimtangulia akiwahubiria watu wote wa Israeli kwamba ni lazima watubu na kubatizwa. 25Yohane alipokuwa anamaliza ujumbe wake aliwaambia watu: Mnadhani mimi ni nani? Mimi si yule mnayemtazamia. Huyo anakuja baada yangu na mimi sistahili hata kuzifungua kamba za viatu vyake.

26Ndugu, ninyi mlio watoto wa ukoo wa Abrahamu, na wengine wote mnaomcha Mungu! Ujumbe huu wa wokovu umeletwa kwetu. 27Kwa maana wenyeji wa Yerusalemu na wakuu wao hawakumtambua yeye kuwa Mwokozi. Wala hawakuelewa maneno ya manabii yanayosomwa kila Sabato. Hata hivyo, waliyafanya maneno ya manabii yatimie kwa kumhukumu Yesu adhabu ya kifo. 28Ingawa hawakumpata na hatia inayostahili auawe, walimwomba Pilato amhukumu auawe. 29Na baada ya kutekeleza yote yaliyokuwa yameandikwa kumhusu yeye, walimshusha kutoka msalabani, wakamweka kaburini. 30Lakini Mungu alimfufua kutoka wafu. 31Naye, kwa siku nyingi aliwatokea wale waliofuatana naye kutoka Galilaya mpaka Yerusalemu. Hao ndio walio sasa mashahidi wake kwa watu wa Israeli. 32Sisi tumekuja hapa kuwaleteeni Habari Njema: jambo lile Mungu alilowaahidia babu zetu amelitimiza sasa kwa ajili yetu sisi tulio wajukuu wao kwa kumfufua Yesu kutoka wafu. 33Kama ilivyoandikwa katika zaburi ya pili: Wewe ni Mwanangu, mimi leo nimekuwa baba yako. 34Na juu ya kumfufua kutoka wafu, asipate tena kurudi huko na kuoza, Mungu alisema hivi: Nitakupa baraka takatifu na za kweli nilizomwahidia Daudi. 35Naam, na katika sehemu nyingine za zaburi asema: Hutamwacha Mtakatifu wako aoze. 36Sasa, Daudi mwenyewe alitimiza mapenzi ya Mungu wakati wake; kisha akafa na kuzikwa karibu na wazee wake, na mwili wake ukaoza. 37Lakini yule ambaye Mungu alimfufua kutoka wafu hakupata kuoza. 38Jueni wazi, ndugu zangu, kwamba ujumbe kuhusu kusamehewa dhambi unahubiriwa kwenu kwa njia ya Yesu Kristo; 39na ya kwamba kila mmoja anayemwamini Yesu anasamehewa dhambi zote, jambo ambalo halingewezekana kwa njia ya Sheria ya Mose. 40Jihadharini basi, msije mkapatwa na yale yaliyosemwa na manabii:

41Sikilizeni enyi wenye madharau, shangaeni mpotee! Kwa maana kitu ninachofanya sasa, nyakati zenu, ni kitu ambacho hamtakiamini hata kama mtu akiwaelezeni."

42Paulo na Barnaba walipokuwa wanatoka katika ile sunagogi, wale watu waliwaalika waje tena siku ya Sabato iliyofuata, waongee zaidi juu ya mambo hayo. 43Mkutano huo ulipomalizika, Wayahudi wengi na watu wa mataifa mengine waliokuwa wameongokea dini ya Kiyahudi waliwafuata Paulo na Barnaba. Hao mitume waliongea nao, wakawatia moyo waendelee kuishi wakitegemea neema ya Mungu.

44Siku ya Sabato iliyofuata, karibu kila mtu katika ule mji alikuja kusikiliza neno la Bwana. 45Lakini Wayahudi walipoliona hilo kundi la watu walijaa wivu, wakapinga alichokuwa anasema Paulo na kumtukana. 46Hata hivyo, Paulo na Barnaba waliongea kwa uhodari zaidi, wakasema, "Ilikuwa ni lazima neno la Mungu liwafikieni ninyi kwanza; lakini kwa kuwa mmelikataa na kujiona hamstahili uzima wa milele, basi, tunawaacheni na kuwaendea watu wa mataifa mengine.

47Maana Bwana alituagiza hivi: Nimekuteua wewe uwe mwanga kwa mataifa, uwe njia ya wokovu kwa ulimwengu wote."

48Watu wa mataifa mengine waliposikia jambo hilo walifurahi, wakausifu ujumbe wa Mungu; na wale waliokuwa wamechaguliwa kupata uzima wa milele, wakawa waumini. 49Neno la Bwana likaenea kila mahali katika sehemu ile. 50Lakini Wayahudi waliwachochea wanawake wa tabaka ya juu wa mataifa mengine ambao walikuwa wacha Mungu, na wanaume maarufu wa mji huo. Wakaanza kuwatesa Paulo na Barnaba, wakawafukuza kutoka katika eneo lao. 51Basi, mitume wakayakung'uta mavumbi yaliyokuwa katika miguu yao kama onyo, kisha wakaenda Ikonio. 52Lakini hao wafuasi walikuwa wamejaa furaha na Roho Mtakatifu.



Public Domain Swahili New Testament -- PLEASE MAKE COPIES FOR YOUR FRIENDS, NO ROYALTY DUE.

Bible Hub

Acts 12
Top of Page
Top of Page