Matayo 22
Swahili NT
1Yesu alisema nao tena kwa kutumia mifano: 2Ufalme wa mbinguni umefanana na mfalme aliyemwandalia mwanawe karamu ya arusi. 3Basi, akawatuma watumishi kuwaita walioalikwa waje arusini, lakini walioalikwa hawakutaka kufika. 4Akawatuma tena watumishi wengine, akisema, Waambieni wale walioalikwa: karamu yangu iko tayari sasa; fahali wangu na ng'ombe wanono wamekwisha chinjwa; kila kitu ni tayari, njoni arusini. 5Lakini wao hawakujali, wakaenda zao; mmoja shambani kwake, mwingine kwenye shughuli zake, 6na wengine wakawakamata wale watumishi wakawatukana, wakawaua. 7Yule mfalme akakasirika, akawatuma askari wake wakawaangamize wauaji hao na kuuteketeza mji wao. 8Kisha akawaambia watumishi wake: Karamu ya arusi iko tayari kweli, lakini walioalikwa hawakustahili. 9Basi, nendeni kwenye barabara na wowote wale mtakaowakuta waiteni waje arusini. 10Wale watumishi wakatoka, wakaenda njiani, wakawaleta watu wote, wabaya na wema. Nyumba ya arusi ikajaa wageni.

11Mfalme alipoingia kuwaona wageni, akamwona mtu mmoja ambaye hakuvaa mavazi ya arusi. 12Mfalme akamwuliza, Rafiki, umeingiaje hapa bila vazi la arusi? Lakini yeye akakaa kimya. 13Hapo mfalme akawaambia watumishi, Mfungeni miguu na mikono mkamtupe nje gizani; huko atalia na kusaga meno." 14Yesu akamaliza kwa kusema, "Wengi wamealikwa, lakini wachache wameteuliwa."

15Kisha, Mafarisayo wakaenda zao, wakashauriana jinsi ya kumnasa Yesu kwa maneno yake. 16Basi, wakawatuma wafuasi wao pamoja na wafuasi wa kikundi cha Herode. Wakamwuliza, "Mwalimu, tunajua kwamba wewe ni mtu mwaminifu, na kwamba wafundisha njia ya Mungu kwa uaminifu; humwogopi mtu yeyote, maana cheo cha mtu si kitu kwako. 17Haya, twambie maoni yako. Je, ni halali au la, kulipa Kaisari?" 18Lakini Yesu alitambua uovu wao, akawaambia, "Enyi 19Nionyesheni fedha ya kulipia kodi." Nao wakamtolea sarafu ya fedha. sarafu ya fedha. 20Basi, Yesu akawauliza, "Sura na chapa hii ni ya nani?" 21Wakamjibu, "Ni vya Kaisari." Hapo Yesu akawaambia, "Basi, mpeni Kaisari yaliyo yake Kaisari, na Mungu yaliyo yake Mungu." 22Waliposikia hivyo wakashangaa; wakamwacha, wakaenda zao.

23Siku hiyo, baadhi ya Masadukayo walimwendea Yesu. Hao ndio wale wasemao kwamba wafu hawafufuki. 24Basi, wakamwambia, "Mwalimu, Mose alisema mtu aliyeoa akifa bila kuacha watoto, lazima ndugu yake amwoe huyo mama mjane, amzalie ndugu yake watoto. 25Sasa, hapa petu palikuwa na ndugu saba. Wa kwanza alioa kisha akafa bila kujaliwa watoto, akamwachia ndugu yake huyo mke wake mjane. 26Ikawa vivyo hivyo kwa ndugu wa pili, na wa tatu, mpaka wa saba. 27Baada ya ndugu hao wote kufa, akafa pia yule mama. 28Je, siku wafu watakapofufuka mama huyo atakuwa mke wa nani miongoni mwa wale ndugu saba? Maana Wote saba walimwoa."

29Yesu akawajibu, "Kweli mmekosea kwa sababu hamjui Maandiko Matakatifu wala nguvu ya Mungu! 30Maana wafu watakapofufuliwa hawataoa wala kuolewa, watakuwa kama malaika mbinguni. 31Lakini kuhusu suala la wafu kufufuka, hamjasoma yale aliyowaambieni Mungu? 32Aliwaambia, Mimi ni Mungu wa Abrahamu, Isaka na Yakobo! Basi, yeye si Mungu wa wafu, bali ni Mungu wa walio hai." 33Ule umati wa watu uliposikia hivyo ukayastaajabia mafundisho yake.

34Mafarisayo waliposikia kwamba Yesu alikuwa amewanyamazisha Masadukayo, wakakutana pamoja. 35Mmoja wao, mwanasheria, akamwuliza Yesu kwa kumjaribu, 36Mwalimu, ni amri ipi iliyo kuu katika Sheria ya Mose? 37Yesu akamjibu, "Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote na kwa akili yako yote. 38Hii ndiyo amri kuu ya kwanza. 39Ya pili inafanana na hiyo: Mpende jirani yako kama unavyojipenda wewe mwenyewe. 40Sheria yote ya Mose na mafundisho ya manabii vinategemea amri hizi mbili."

41Mafarisayo walipokusanyika pamoja, Yesu aliwauliza, 42Ninyi mwaonaje juu ya Kristo? Je, ni mwana wa nani? Wakamjibu, "Wa Daudi." 43Yesu akawaambia, "Basi, inawezekanaje kwamba kwa nguvu ya Roho Mtakatifu Daudi anamwita yeye Bwana? Maana alisema:

44Bwana alimwambia Bwana wangu: keti upande wangu wa kulia, mpaka niwaweke adui zako chini ya miguu yako.

45Basi, ikiwa Daudi anamwita Kristo Bwana, anawezaje kuwa mwanawe?" 46Hakuna mtu yeyote aliyeweza kumjibu neno. Na tangu siku hiyo hakuna aliyethubutu tena kumwuliza swali.



Public Domain Swahili New Testament -- PLEASE MAKE COPIES FOR YOUR FRIENDS, NO ROYALTY DUE.

Bible Hub

Matthew 21
Top of Page
Top of Page